Tuesday, November 21, 2017

UJENZI MAGOMENI KOTA KUKAMILIKA MACHI MWAKANI

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Mhe. Elias Kwandikwa (katikati), akitoa maelekezo kwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Msanifu Majengo Elius Mwakalinga (kulia) wakati akikagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi eneo la Magomeni Kota jijini Dar es Salaam.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Msanifu Majengo Elius Mwakalinga (kulia) akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Mhe. Elias Kwandikwa (katikati), kuhusu hatua zilizofikiwa katika utelezaji wa mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi eneo la Magomeni Kota, wakati akikagua maendeleo ya ujenzi huo, jijini Dar es Salaam.
Muonekano wa mtambo wa kuchakata zege unaotumiwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), katika mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi eneo la Magomeni Kota, jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Mhe. Elias Kwandikwa, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani), mara baada ya kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi eneo la Magomeni Kota, jijini Dar es Salaam.
Muonekano wa baadhi ya vitalu vya makazi eneo la Magomeni Kota zinazojengwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 35.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Mhe. Elias Kwandikwa, akizungumza na menejimenti ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), wakati alipowatembelea wakala huo leo, jijini Dar es Salaam.
Meneja Rasilimali Watu kutoka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Bi. Gerwalda Luoga, akitoa neno la shukrani kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Mhe. Elias Kwandikwa (hayupo pichani) mara baada ya kikao kazi na Naibu Waziri huyo, jijini Dar es Salaam.


Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mheshimiwa Elias Kwandikwa (Mb), ameutaka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), kufanya kazi kwa bidii katika miradi yote inayopewa na Serikali ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati na ubora unaotakiwa.

Akikagua hatua zilizofikiwa katika mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi eneo la Magomeni kota, Naibu Waziri Kwandikwa, amesema kuwa Serikali itaendelea kuanisha miradi mingine ili kuhakikisha fedha za Serikali zinaokolewa na kusimamiwa kwa uzalendo.

“Hakikisheni mnafanya kazi zenu kwa weledi, uzalendo na kukamilisha miradi kwa wakati na kuokoa fedha ambazo zitatumika katika utekelezaji wa miradi mingine hapa nchini”, amesisitiza Mhe. Kwandikwa.

Ametoa wito kwa wataalamu wengine kuja kupata mafunzo kwa TBA ambao ni chachu ya utekelezaji wa miradi mingi hapa nchini kwa kuwa wanatumia mfumo wa kisayansi na mitambo yenye kusaidia kupunguza gharama za ujenzi.

Aidha, Naibu Waziri huyo ameushukuru uongozi wa TBA kwa kutoa ajira za vibarua takribani 200 kwa siku katika mradi huo na kuwataka wafanyakazi hao kuwa waadilifu na waaminifu ili kuwa na sifa za kupata ajira za kudumu.

Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Msanifu Majengo Elius Mwakalinga, amemhakikishia Naibu Waziri Kwandikwa kukamilika mradi huo kwa wakati, ubora na kwa gharama nafuu.

Amefafanua kuwa mradi huo utakuwa una jumla ya vitalu vitano ambapo vitalu vinne vina majengo ya ghorofa nane na kitalu kimoja kina jengo la ghorofa tisa na hivyo mradi utatoa makazi kwa kaya 656.

Mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi eneo la Magomeni Kota unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Machi mwakani na utagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 20 zote ikiwa ni fedha za Serikali.

No comments: