Friday, June 30, 2017

Viongozi wa Dini kanda ya Ziwa Wabebeshwa mzigo, Utunzaji wa Mazingira Ziwa Victoria

Mkuu wa mkoa wa Mara Dkt. Charles Mlingwa, akifungua kikao hicho, pembeni kulia ni Mratibu wa LVEMP Bw. Omari Myanza.
Na Atley Kuni,  Mwanza.

Serikali mkoani hapa, imewapa jukumu kubwa viongozi wa dini kutoka baadhi ya mikoa ya kanda ya ziwa kuhakikisha wanakuwa bega kwa bega katika kulitunza ziwa Viktoria na Maliasili zake ili liweze kuwa tegemeo kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Akifungua Semina ya siku moja mkoani hapa Mkuu wa mkoa wa Mwanza John Mongella, na risala yake kusomwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara Dkt. Charles Mlingwa, Mongella amesema, viongozi wa dini wanalo jukumu kubwa kwani wao husimamia imani za watu.
Baba Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo katoliki Musoma Mkoani Mara akiongea na Waandishi wa habari nje ya Mkutano huo kuelezea umuhimu wa mazingira.

“Ninyi Viongozi wa dini dhima mliyonayo ndani ya jamii ni kubwa sana na chochote mtakacho waelekeza waumini wenu lazima waweze kukitekeleza, hivyo niwaombe sana viongozi wangu tulilinde ziwa viktoria kwa jitihada zetu zote’’ alisema Mongella.

Aidha Mongella amesema kuwa, kuwepo kwa Ziwa Victoria ni fursa ya uendelezaji ya kauli mbiu ya “Tanzania ya Viwanda” ambayo Serikali ya awamu ya Tano inasisitiza, “Ziwa hili linasaidia upatikanaji wa rasilimali zinazotumika kwa matumizi ya nyumbani na viwandani, usafiri na usafirishaji na uzalishaji wa nishati ya umeme Hivyo basi hatuna budi kuhifadhi mazingira ya Ziwa na Bonde lake” amesisitiza Mkuu huyo wa mkoa.

Kwa upande wao, viongozi wa dini wakiongea wamesema, wao wanatambua na hata vitabu vya dini vinaelekeza juu ya mwanadamu anachopaswa kufanya katika kulinda mazingira ikiwepo ziwa Viktoria.
Sheik Hassan Kabeke, akiafafnua jambo kwa waandishi wa habari nje ya Warsha hiyo namna suala la mazingira linavyo tajwa katika Kuran tukufu.

Mwenyekiti mwenza wa Kamati ya amani ya madhehebu ya dini katika Mkoa wa Mwanza, Sheik Hassan Kabeke, amesema katika Uislam na hususan ni katika mafundisho ya Mtume Muhama S.A.W, inafafanua juu ya mito miwili yaani mto Nile na Furabu ambayo mtume aliipitia huku akisema kwamba, Mto Nile ambao unafungamanishwa na Ziwa Viktoria Mtume amesisitiza kuyatunza mazingira, “Katika kupanda miti kwenye uislamu mtu hupata thawabu, tunaimani kabisa kwamba kila mmoja wetu akitunza mazingira ni sehemu ya Ibada, amesema Kabeke.

Naye Baba Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo Katoliki la Musoma, kwa upande wake amesema kwa habari ya mazingira, tunaona ni jukumu la jamii nzima bila kujali itikadi zetu “ Kukutana kwetu hapa tunataka kuangalia nikwa namna gani tutaziangazia sababu za kiuchumi na kijamii, alisema Msonganzila na kuongeza kwamba kwa sasa wao katika Mkoa wa Mara wanayo kampeni kwenye eneo la Serengeti ambayo wanaendelea kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa Utunzaji wa mazingira na mabadiliko ya hali ya nchi.
Mratibu wa LVEM Akitoa maelezo ya awali kabla yakuanza kwa Warsha hiyo ilikutanisha Viongozi wa Serikali na Dini katika baadhi ya Mikoa ya kanda ya ziwa (Picha zote na Ofisi ya mkuu wa Mkoa Mwanza).

Mradi wa Hifadhi ya Mazingira wa Ziwa Victoria (LVEMP II) utakamilika mwezi Disemba, 2017, aidha warsha hiyo ni kati ya warsha nne zilizoandaliwa na Mradi kwa madhumuni ya kukusanya maoni ya wadau ambayo yatawezesha kuandaa awamu ijayo ya Mradi inayotarajiwa kuanza kutekelezwa kuanzia mwaka 2018.

Kikao hicho kimewakutanisha Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa pamoja na Viongozi wa dini kutoka mikoa ya Mwanza, Geita, Kagera, Simiyu na Mara.
Baadhi ya Viongozi wa dini kutoka mkoa wa kagera wakiwa katika Warsha hiyo.

No comments: