Friday, May 19, 2017

Muhimbili: Upungufu wa Wauguzi Kushughulikiwa, Maslahi Kuboreshwa

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa (MNH), Profesa Lawrence Museru akizungumza na wauguzi leo katika maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani ambayo hufanyika Mei 12,kila mwaka.
A
 Baadhi ya Wauguzi wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Profesa Museru katika maadhimisho hayo.
A 1
 Baadhi ya Wauguzi wakirudia kiapo kwamba wataendelea kutoa huduma kwa wagonjwa kwa kuzingatia uadilifu.
A 2
Muuguzi wa Muhimbili, Furaha Tada akitoa mada kwenye maadhimisho hayo leo.
A 3
Wauguzi wakifuatilia mada iliyowasilishwa na mmoja wa wauguzi wa hospitali hiyo.
A 5
Philonem Kaongo ambaye ni Muuguzi Mkunga akitoa mada kwenye maadhimisho.
A 6
Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Profesa Museru akipokea risala kutoka kwa Debora Bukuku baada ya kuisoma kwenye maadhimisho hayo.
 A 7
Katibu Mkuu wa Chama cha Wauguzi Tanzania, Sebastian Luziga akizungumza kwenye maadhimisho hayo leo.
…………………….
Uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), umesema utaendelea kuboresha maslahi ya wafanyakazi wa hospitali hiyo na kushughulikia tatizo la upungufu wa wauguzi.
 
Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Profesa Lawrence Museru ameyasema hayo leo katika maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani, Tawi la Muhimbili ambayo huadhimishwa Mei 12 kila mwaka. Kauli mbiu ya mwaka huu “ Wauguzi Mbiu ya Kufikia Malengo Endelevu ya Milenia.”
 
Profesa Museru amesema Serikali ipo bega kwa bega na hospitali hiyo katika kupata ufumbuzi wa tatizo hilo. “Serikali imeahidi kutatua tatizo la upungufu wa wauguzi katika siku chache zijazo,” amesema Profesa Museru.
 
Amesema uongozi wa hospitali unashughulikia posho za wauguzi na pia 
kuboresha mazingira ya kazi ili wauguzi watoe huduma bora kwa wagonjwa. 
“Pia uongozi wa muhimbili utaendelea kuboresha maslahi ya wafanyakazi ili wafanye kazi wa ufanisi,” amesema Profesa Museru.
 
Awali mwakilishi wa wauguzi, Debora Bukuku alisoma risala ikielezea changamoto mbalimbali zikiwamo mazingira magumu na hatarishi ya kazi na pia kupitia risala hiyo waliomba wapatiwe posho za sare pamoja na kuboreshewa maslahi mengine.
 
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi amewataka madaktari na wauguzi kuendelea kuandika machapisho ambayo yanaeleza mafanikio na changamoto za utoaji huduma zilizopo katika hospitali hiyo.
 
“Bila kuandika machapisho, hakuna atakayeona mafanikio yetu. Hii ni hospitali ya Taifa ambayo inategemewa na hospitali nyingine kujifunza mambo mbalimbali. Hivyo nawapongeza wauguzi kwa kuandaa mada mbambali na kuziwasilisha kwenye maadhimisho ya siku ya wauguzi duniani,” amesema Profesa Museru.
 
Katika kongamano hilo wauguzi na wataalamu wengine waliwasilisha mada mbalimbali kuhusu wanavyotoa huduma mbalimbali kwa wagonjwa na jinsi ya kuboresha huduma kwa wagonjwa wa kansa, figo na kutoa huduma bora kwa wagonjwa wa magonjwa ya dharura na ajali.
 
 Muuguzi Mkunga wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Philomen Kaongo katika kongamano hilo alizungumzia jinsi ya kuzuia na kutibu ugonjwa wa kansa.

No comments: