Tuesday, December 30, 2014

Matukio ya kutishia amani ya nchi na usalama wa raia yatapungua kama mabalozi wa nyumba kumi watafanya kazi zao kwa uaminifu - Vuai Ally Vuai

Na Anna Nkinda – Maelezo, Lindi

Matukio ya kutishia amani ya nchi na usalama wa raia yatapungua kama mabalozi wa nyumba kumi watafanya kazi zao kwa uaminifu kwani wao ni viongozi wa kwanza walio karibu na wananchi hivyo basi wanatakiwa kuwafahamu wakazi wa maeneo yao.

Hayo yamesemwa jana na Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Vuai Ally Vuai wakati akifungua semina ya siku moja ya  uwezeshaji wa chama hicho kwa  mabalozi (viongozi wa mashina) wa wilaya ya Lindi mjini.

Vuai alisema Balozi ni kiongozi wa kwanza anayetakiwa kujua idadi ya wakazi wake, kazi wanazozifanya na majina yao kitendo ambacho kitasaidia kuimarisha usalama wa eneo husika lakini miaka ya hivi karibuni wameacha kufanya kazi hiyo kwa uadilifu na kuviachia vyombo vya dola pekee.

“Jukumu la kulinda amani ya nchi na usalama wa taifa letu ni la kila mtu, lakini hivi sasa kazi hiyo vimeachiwa vyombo vya dola pekee, mabalozi fanyeni kazi ya kuwatambua wakazi wa maeneo mnayoishi hii itasaidia kumtambua mualifu pale atakapofika katika eneo lenu”, alisema Vuai.

Alisema kikao cha kwanza cha CCM ni kikao cha shina hivyo basi mabalozi ni viongozi wa muhimu ndani ya shina wanatakiwa kutetea ilani ya uchaguzi ya mwaka 2010 na kutowaachia viongozi wakuu wa chama pekee kufanya kazi hiyo.

Vuai alisisitiza, “Muwe na uthubutu wa kujibu hoja potofu za wapinzani na kutokubali wawapotoshe wananchi juu ya mafanikio yaliyofanywa na Serikali. Kipindi cha uchaguzi kikifika endeleeni kuwahimiza na kuwasimamia wananchi wakapige kura ili wasipoteze haki yao ya msingi ya kupiga kura”.

Aliwataka mabalozi hao kuhakikisha wakati wa kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi mkuu utakaofanyika hapo mwakani wawahimize  wananchi ili waweze kujitokeza kwa wingi kujiandikisha majina yao.

Kwa upande wake Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM kupitia wilaya ya Lindi mjini Mama Salma Kikwete alisema mabalozi ni msingi na nguzo ya chama bila ya mabalozi chama hakiwezi kwenda vizuri ni kama vile binadamu anaweza kuwa na kila kitu lakini kama hana miguu hawezi kutembea.

Aliwapongeza kwa ushindi walioupata wakati wa uchaguzi wa Wenyeviti na Wajumbe wa Serikali za mitaa na kusema kuwa upendo na mshikamano ni msingi wa ushindi na usiri na uadilifu ni nyenzo muhimu katika utendaji wao wa kazi.

“Katika semina hii mtafundishwa mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kazi na wajibu wenu kwa Chama na Jamii inayowazunguka hivyo basi muwe wasikivu na kuyashika yale mtakayofundishwa na watoa mada”, alisisitiza Mama Kikwete.

Akiongea kwa niaba ya wajumbe walioshiriki semina hiyo Rashid Thabit kutoka kata ya Rahaleo alishukuru kwa mafunzo waliyoyapata na kusema kuwa yatawasaidia katika utendaji wao wa kazi.

“Tunakushukuru MNEC kwa ajili ya kuandaa mafunzo haya ambayo yametupa uelewa na wajibu na kazi zetu kama mabalozi. Uwepo wako wakati wa uchaguzi uliopita ulitufanya tukashinda kwani tulishiriki pamoja nawe katika kampeni za kuwanadi wagombea wetu”.

Nawaomba wajumbe wenzangu tusibweteke na ushindi huu bali tuongeze kasi na bidii na kuweza kufanya vizuri katika uchaguzi mkuu utakaofanyika hapo mwakani ili tuweze kulikomboa jimbo la Lindi mjini kutoka mikononi mwa Chama Cha Wananchi (CUF)”, alisema Thabit.

Semina hiyo ya siku moja iliyohudhuriwa na wajumbe 993 kutoka kata zote 18 za wilaya hiyo iliandaliwa na Mama Kikwete ambaye aliwaahidi mabalozi kuwapa mafunzo hayo ili wajue majukumu yao ya kazi. Mada zilizojadiliwa ni kazi na wajibu wa mabalozi na katiba mpya iliyopendekezwa.

No comments: