Saturday, January 21, 2017

MAGAZETI YA LEO JUMAMOSI JANUARI 21, 2017


Taarifa kwa umma kuhusu ziara ya Rais wa Uturuki nchini

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI


Description: Coat of Arms

Simu: 255-22-2114615, 211906-12
Barua pepe: nje@nje.go.tz
Barua pepe: gcu@nje.go.tz

Nukushi: 255-22-2116600

              

               20 KIVUKONI FRONT,
                          P.O. BOX 9000,
                 11466 DAR ES SALAAM,  
                                   Tanzania.
Rais wa Jamhuri ya Uturuki, Mheshimiwa Recep Tayyip Erdogan anatarajiwa kufanya ziara ya kitaifa ya siku mbili nchini tarehe 22 na 23 Januari 2017 kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Mhe. Rais Erdogan ambaye ataambatana na Mkewe, na kuongoza ujumbe wa watu 150 wakiwemo Mawaziri, Wabunge, Maafisa kutoka Serikalini na Wafanyabiashara anatarajiwa kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere tarehe 22 Januari, 2017 jioni  na atapokelewa na Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Madhumuni ya ziara hiyo ni kukuza mahusiano mazuri yaliyopo baina ya Uturuki na Tanzania pamoja ‎na kupanua fursa za uwekezaji hususan katika maeneo ya biashara  na uwekezaji.
Wakati wa ziara hiyo, Mhe. Erdogan  atakutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa mazungumzo ya faragha yatakayofuatiwa  na mazungumzo rasmi yatakayowahusisha wajumbe wa pande mbili na baadaye Marais hao watashuhudia uwekwaji saini wa mikataba ya ushirikiano kwenye maeneo mbalimbali.
Siku hiyo ya tarehe 23 Januari, 2017, kutakuwa na Kongamano la Biashara kati ya Uturuki na Tanzania litakalowakutanisha Wafanyabiashara kutoka nchi hizi mbili. Kongamano hilolitahutubiwa na viongozi wa Tanzania na Uturuki.
Mhe. Rais Erdogan na ujumbe wake watashiriki Dhifa ya Chakula cha jioni kilichoandaliwa Ikulu kwa heshima yake na Mhe. Rais Magufuli.
Mahusiano ya Uturuki na Tanzania
Mahusiano ya Tanzania na Uturuki ni mazuri. Ikumbukwe kuwa, kufunguliwa kwa mara nyingine kwa Ubalozi wa Uturuki hapa nchini mnamo Mei 2009 kuliongeza kasi ya mahusiano baina ya nchi hizi mbili.  Tangu kipindi hicho kumekuwa na ziara za viongozi wa kitaifa wa nchi hizi mbili ili kukuza na kudumisha mahusiano. Katika hatua nyingine Tanzania imetangaza kufungua Ubalozi wake nchini Uturuki na hivi leo Mhe. Rais atamwapisha Balozi Mteule, Prof. Elizabeth Kiondo atakayetuwakilisha Uturuki.
Pia kumekuwa na ziara za viongozi wakuu wa kitaifa wa nchi hizi mbili ikiwemo ziara ya Rais mstaafu wa Uturuki, Mhe. Abdullah Gul  nchini mwaka 2009 ; ziara ya Rais wa Awamu ya Nne wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete nchini Uturuki mwaka 2010 na ziara ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein mwaka 2011.
Tume ya Pamoja ya Biashara
Tanzania na Uturuki zinashirikiana pia kupitia Tume ya Pamoja ya Biashara ambayo ilianzishwa baada ya kusainiwa kwa Mkataba wa Ushirikiano kwenye masuala ya Biashara mwaka 2010. Kikao cha kwanza cha Tume hiyo kilifanyika Jijini Dar es Salaam mwezi Novemba 2012. Katika kikao hicho pande zote zilikubaliana kushirikiana kwenye maeneo mbalimbali hususan biashara na uwekezaji, elimu, Kilimo, Nishati na Madini, Maendeleo ya viwanda na mawasiliano ya simu.
Kikao cha Pili cha Tume ya Pamoja ya Biashara kati ya Tanzania na Uturuki kilifanyika tarehe 11 – 12 Januari 2017, Uturuki kwa lengo la kujadili utekelezaji wa Makubaliano ya Kikao cha Kwanza na kuibua maeneo mapya ya ushirikiano kati ya pande hizi mbili. Aidha, Mkutano huu pia ulikuwa na umuhimu wa kipekee kwa kuwa ulifanyika ikiwa ni maandalizi ya ziara ya Kiserikali ya Mheshimiwa Recep Tayyip Erdo─čan, Rais wa Jamhuri ya Uturuki inayotarajiwa kufanyika tarehe 23 Januari, 2017.
Pande zote mbili zimekubaliana kuongeza nguvu katika kuhamasisha uwekezaji kwenye nchi zetu. Katika kutekeleza hili, Uturuki imepanga kuandaa Mkutano wa Uwekezaji kati ya Tanzania na Uturuki ndani ya robo ya pili ya mwaka huu jijini Istanbul. Vile vile, nchi zote mbili zimekubaliana kubadilishana taarifa za fursa za uwekezaji kupitia Balozi zetu na Baraza la Biashara la Tanzania na Uturuki. Aidha, Taasisi zetu za Uwekezaji zimeelekezwa kuanza majadiliano ya kuingia Mkataba wa Ushirikiano ili kuhamasisha uwekezaji nchini. Hali kadhalika, Uturuki imemchagua Mwambata wa Biashara katika Ubalozi wao wa Dar es Salaam na Tanzania imeahidi kuteua Afisa Maalum ndani ya mwezi mmoja kushughulikia uhamasishaji wa uwekezaji na biashara kati ya nchi hizi mbili.
Mafanikio yaliyopatikana kutokana na ushirikiano kati ya Tanzania na Uturuki
Tangu kuanzishwa kwa Tume ya pamoja ya ushirikiano ya kiuchumi mafanikio ya ushirikiano baina ya nchi hizi mbili yameonekana ikiwemo:- Kuimarishwa kwa ushirikiano katika masuala ya Usafiri wa Anga ambapo Shirika la Ndege la Uturuki lilianzisha safari tatu  za moja kwa moja kutoka Istanbul hadi Dar es Salaam, Kilimanjaro na hivi karibuni Zanzibar. Kuanzishwa kwa safari hizi kumekuza biashara kati ya Uturuki na Tanzania  ambapo mwaka 2009  ukubwa wa biashara ulikuwa Dola za Marekani milioni 66 sawa na shilingi bilioni 145.2 lakini hadi kufikia Februari 2016 biashara kati  ya nchi hizi mbili iliongezeka kwa Dola za Kimarekani milioni 160 sawa na shilingi bilioni 352.
Aidha, kuzinduliwa kwa Baraza la Biashara kati ya Tanzania na Uturuki mwaka 2013 ambalo kumewezesha kuimarisha ushirikiano wa sekta binafsi za nchi hizi mbili na  Kuongezeka kwa Makampuni ya Uturuki yaliyowekeza nchini ambapo hadi sasa ni Kampuni 30 zimefanya uwekezaji wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 305.08 na zinatarajiwa kutengeneza ajira 2,959.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dar es Salaam
20 Januari, 2017

Friday, January 20, 2017

DENMARK KUHAMASISHA WAWEKEZAJI KUJA KUWEKEZA TANZANIA

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (wa kwanza kulia), akisisitiza jambo wakati wa mkutano wake na ujumbe kutoka nchini Denmark, ukiongozwa na Waziri wa nchi anayeshughulikia Sera, Bw. Martin Hermann, walipokutana Makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es salaam.
Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango na Ujumbe kutoka Serikali ya Denmark ukiongozwa na Waziri wa Nchi-Sera, Bw. Martin Hermann, walipokutana kwa mazungumzo kuhusu ushirikiano kati ya nchi hizo mbili, Mkutano uliofanyika Makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es salaam.
Waziri wa Nchi anayehusika na masuala ya Sera, Bw. Martin Hermann (kulia) akiwa na ujumbe wake wakati wa mazungumzo kati yake na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (hayupo pichani), Makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es salaam, ambapo nchi hizo zimekubaliana kuendeleza ushirikiano utakaojikita katika masuala ya uwekezaji na biashara kwa faida ya pande zote mbili. Kushoto ni Balozi wa Denmark hapa nchini Bw. Einar Jansen.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (kushoto), akisisitiza jambo wakati wa mkutano wake na ujumbe kutoka nchini Denmark, ukiongozwa na Waziri wa nchi anayeshughulikia Sera, Bw. Martin Hermann, (hayupo Pichani) walipokutana Makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es salaam. Kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji (kulia) na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw. Doto James, wakifuatilia kwa umakini mazungumzo kati ya Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango na Waziri wa Nchi anayeshughulika na masuala ya Sera wa Denmark, Bw. Martin Hermann (hawapo pichani), Makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es salaam.
Waziri wa Nchi anayehusika na masuala ya Sera kutoka Denmark, Bw. Martin Hermann (kushoto) akimkabidhi Dkt. Mpango, nyaraka za kampuni zinazoonesha nia ya kuwekeza Tanzania katika Sekta ya Gesi na Mafuta wakati akiongoza ujumbe wa nchi hiyo katika mazungumzo kati yake na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (kulia), Makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es salaam.


Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango (katikati) akiangalia nyaraka alizokabidhiwa na Waziri wa Nchi wa Serikali ya Denmark anayehusika na Sera, Bw. Martin Hermann, wakati wa mazungumzo kati yao yaliyojikita katika masuala ya kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kati ya nchi hizo mbili. Kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw. Doto James na kulia kwa Waziri Dkt. Mpango, ni Naibu Katibu Mkuu Dkt. Khatib Kazungu.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (wa pili kushoto) akiwa na wageni wake kutoka Serikali ya Denmark wakiongozwa na Waziri wa Nchi anayehusika na Sera, Bw. Martin Hermann (kushoto), baada ya kumalizika kwa mazungumzo kati yao ambapo masuala kadhaa yamejadiliwa ikiwemo kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kijamii hususan katika uwekezaji na biashara, mazungungo yaliyofanyika Makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (kushoto) akipeana mkono wa shukurani na mgeni wake kutoka Serikali ya Denmark, Waziri wa Nchi anayehusika na Sera, Bw. Martin Hermann (kushoto), baada ya kumalizika kwa mazungumzo kati yao yaliyogusa Nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijamii hususan katika uwekezaji na biashara, mazungunzo yaliyofanyika makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (kushoto) akiwasindikiza wageni wake kutoka nje ya jengo la Makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es salaam baada ya kumalizika kwa mazungumzo kati ya ujumbe wa Serikali ya Denmark na Tanzania uliolenga kuimarisha uhusiano katika masuala ya uwekezaji na biashara.


(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WFM).


……………….Na Benny Mwaipaja, WFM, Dar es salaam


SERIKALI ya Denmark imeahidi kuwashawishi wawekezaji wakubwa kutoka nchini humo kuja kuwekeza hapa nchini katika sekta za Kilimo, Mifugo, Uvuvi, Viwanda, Bandari, Gesi na Mafuta.


Ahadi hiyo imetolewa Jijini Dar es salaam na Waziri wa Nchi wa Serikali ya Denmark anayeshughulikia Sera, Bw. Martin Hermann, alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, Makao Makuu ya Wizara hiyo.


Bw. Hermann alielezea kufurahishwa kwake na namna Serikali ya Awamu ya Tano ilivyojipanga kuwatumikia wananchi wake kwa kuwaletea maendeleo ya haraka ya kiuchumi pamoja na kuimarisha uwajibikaji, mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi, na kusema kuwa nchi yake inaunga mkono juhudi hizo.


Alisema kuwa nchi yake itasaidia juhudi hizo kwa kuzishawishi kampuni kubwa zenye mitaji na uwezo wa kiteknolojia kutoka sekta binafsi ili zije ziwekeze hapa nchini na hivyo kushiriki katika kukuza uchumi wa nchi.


Amesisitiza pia umuhimu wa serikali kuwekeza juhudi kubwa katika kuendeleza kilimo kwa kuwa sekta hiyo inaweza kuchochea na kutoa mchango mkubwa na wa haraka wa ustawi na maendeleo ya wananchi.


Aidha, Bw. Hermann, ambaye aliambatana na Balozi wa Denmark hapa nchini, Bw. Einar Jensen, amesifu utendaji mzuri wa Rais Mhe. Dkt. John Magufuli katika mapambano dhidi ya vitendo vya ufisadi ikiwemo rushwa na kuishauri Serikali kuweka mfumo wa vita hiyo utakaokuwa endelevu.


Kwa upande wake Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, alisema Serikali inathamini mchango mkubwa wa Denmark katika kukuza uchumi na maendeleo ya Taifa kwa ujumla kwa kusaidia miradi ya maendeleo na ushauri wa kisera.


“Katika kipindi cha zaidi ya miaka 50 ya uhusiano kati ya nchi hizi mbili tumeshuhudia Serikali ya Denmark ikichangia maendeleo yetu katika nyanja zinazokwenda sambamba na vipaumbele vya maono ya mipango yetu ya maendeleo katika sekta za fedha, miundombinu, kilimo, afya na elimu”alisisitiza Dkt. Mpango.


Dkt. Mpango aliishauri nchi hiyo kwamba mwelekeo wa uhusiano huo sasa uwe katika kushirikiana kiuchumi kwa kuhamasisha uwekezaji na biashara kati ya pande hizo mbili.


Alifafanua kuwa amejaribu kutafuta takwimu za kiwango cha uagizaji na uingizaji wa bidhaa kati ya Tanzania na Denmark lakini cha kusikitisha hakuna biashara hiyo jambo ambalo amesema inabidi lilisisitizwe katika mfumo mpya wa ushirikiano kwa kuwa kuna fursa nyingi zinazoweza kusaidia pande zote mbili kiuchumi.


Alisisitiza kuwa mwelekeo huo ni muhimu utiliwe mkazo sambamba na jitihada za Serikali za kuboresha mazingira ya kufanya biashara na kuwekeza hapa nchini huku akitoa wito kwa kampuni za Denmark zilizopo hapa nchini pia kuvuta kampuni nyingine kutoka nchini mwao kuja kuwekeza Tanzania.


Dkt. Mpango, amewakaribisha wawekezaji hao kuwekeza katika katika sekta za ufugaji wa samaki, ujenzi wa viwanda vya kuchakata samaki, ufugaji wa ng’ombe wa kisasa na viwanda vya kusindika nyama na maziwa, hatua itakayo saidia kukuza mitaji, kuongeza tija katika sekta hizo na ajira kwa kundi kubwa la vijana.


Kuhusu ushauri uliotolewa na Waziri wa nchi wa Denmark anaye shughulikia Sera, Bw. Martin Hermann wa kujenga mfumo endelevu wa kupambana na rushwa na ufisadi, Dkt. Mpango amesema kuwa Serikali imeanzisha mahakama maalumu ya mafisadi ambayo anaamini ni moja ya ujenzi wa mifumo hiyo endelevu ya kupambana na vitendo hivyo.

SKIPPERS HAVEN: HOTELI ILIYOSHEHENI MICHEZO LULUKI YA BAHARINI

 Na Jumia Travel Tanzania
Unaweza usiamini kwamba ile michezo ya baharini unayoiona kupitia kwenye runinga, wazungu wakiicheza unaweza ukaifanya ukiwa hapahapa nchini Tanzania. Jumia Travel (www.travel.jumia.com) ingependa kukujuza kuwa hoteli ya Skipper’s Haven iliyopo Temeke jijini Dar es Salaam, inayo michezo kadhaa ya baharini ambayo itakustaajabisha.

Hoteli hii ya kifahari na ya kuvutia inapatikana katika peninsula ndogo huku ikiwa na ufukwe binafsi na kukupatia fursa ya kufurahia michezo mbalimbali ya baharini kama ifuatavyo: 


Uvuvi kwenye kina kirefu
Skipper’s Haven ni hoteli pekee katika fukwe za Kusini, iliyopo umbali wa kilometa 40 Kusini mwa Dar es Salaam, yenye vifaa vya kutosha kwa ajili ya uvuvi wa kwenye kina kirefu. Ina wataalamu wenye uzoefu wa muda mrefu na ufukwe unaopendekezwa kuwa bora kwa shughuli hizo katika ukanda wa Afrika ya Mashariki.  


 Kupiga mbizi
Ni ndoto ya kila mpiga mbizi kupata fursa ya kuzamia kwenye kina kirefu cha bahari ya Hindi kujionea utajiri wa viumbe vilivyomo ndani yake. Fukwe za pwani ya Afrika ya Mashariki zinazo aina mbalimbali za samaki na miamba ya kuvutia. Hoteli hii ina vifaa vya kisasa pamoja na wataalamu wa kukusaidia kulifanikisha hilo. Samaki kama vile kobe wa baharini, dolfini na aina kadhaa za nyangumi wanaweza kuonekana kwa urahisi.  

Kusafiri kwenye Jahazi
Mojawapo ya vitu utakavyovikumbuka ukiwa hapa ni pamoja na kusafiri kwenye Jahazi siku nzima ukiwa baharini. Wataalamu waliobobea watakuzungusha sehemu mbalimbali baharini ukiwa kwenye chombo hicho na kufurahia mawimbi ya bahari ya Hindi. 

Michezo ya kwenye maji
Skipper’s Haven inakupatia uzoefu wa aina yake kwa michezo mbalimbali ya kwenye bahari. Michezo kama vile kuelea kwenye puto la plastiki au kuvutwa kwa kutumia boti pamoja na kuelea juu ya maji kwa kutumia kifaa maalumu. Mtu mwenye uzoefu wa yoyote anaweza kushiriki kwani kutakuwa na wataalamu watakaokuwa wanatoa muongozo ili uweze kujifunza na kufurahia.

Kujionea ndege wa aina mbalimbali
Mbali na michezo ya baharini, Skipper’s Haven ni mojawapo ya hoteli zilizojengwa kwa kuzingatia ustawi wa mimea na wanyama kwani hakuna miti iliyokatwa wakati inajengwa. Ukiwa hapa utapata fursa ya kujionea aina tofauti za ndege wakirandaranda na kuruka karibu na eneo hili. Hivyo, kwa wanaopenda kuona ndege wa mwituni ni vizuri kujaribu kutembelea. 

Hoteli hii pamoja na zingine kama vile Jangwani Sea Breeze Resort na Golden Tulip Hotel za jijini Dar es Salaam; Mermaids Cove Beach Resort & Spa, Paradise Beach Resort na Golden Tulip Zanzibar Boutique Hotel za visiwani Zanzibar; Nashera Hotel ya Morogoro na Kwetu Hotel inayopatikana mkoani Tanga zinapatikana kupitia mtandao wa Jumia Travel (www.travel.jumia.com) ambapo kila siku ya Jumatano hutoa punguzo kubwa la bei kwa wateja, zoezi ambalo hudumu mpaka Ijumaa ya kila wiki.

SACCOS YA POLISI YAJIVUNIA MAFANIKIO YA MIAKA KUMI

 Mwenyekiti wa bodi ya chama cha ushirika cha kuweka akiba na kukopa cha Usalama wa Raia Saccos (URA SACCOS LTD) Kamishna wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji (CGF) Thobias E.M. Andengenye (aliyesimama) akitoa neno mbele ya wajumbe wa mkutano mkuu wa  nane (hawapo pichani) wakati wa ufunguzi wa mkutano huo mkoani morogoro jana kulia ni Kaimu Mrajis wa vyama vya Ushirika nchini Bwana Tito Haule, anayefuata ni Makamu Mwenyekiti Kamishna Albert M. Nyamhanga na Kaimu kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro, (ACP) Leonce Rwegasila.
 Wajumbe wa mkutano mkuu wa nane wa chama cha ushirika cha kuweka akiba na kukopa cha Usalama wa Raia Saccos (URA SACCOS LTD), wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi wa mkutano huo Kaimu Mrajis wa vyama vya ushirika nchini Bwana Tito Haule, (hayupo pichani) wakati wa ufunguzi wa mkutano huo uliofanyika jana mkoani Morogoro.
Kaimu Mrajis wa vyama vya ushirika nchini Bwana Tito Haule, pamoja na viongozi wa bodi na wajumbe wa chama cha ushirika cha kuweka akiba na kukopa cha Usalama wa Raia Saccos (URA SACCOS LTD) wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya ufunguzi wa mkutano mkuu wa nane uliofanyika jana mkoani morogoro. (Picha zote na Demetrius Njimbwi – Jeshi la Polisi)

Na Demetrius Njimbwi – Jeshi la Polisi Morogoro
Chama cha ushirika cha kuweka akiba na kukopa cha Usalama wa Raia Saccos (URA SACCOS LTD), kimeendelea kujizolea mafanikio makubwa kwa muda wa miaka kumi toka kuanzishwa kwake huku kikijivunia kukopesha wanachama wake jumla ya fedha taslimu bilioni 113.7

Hayo yamethibitishwa na kaimu Mrajis wa vyama vya ushirika nchini Bwana Tito Haule, wakatia akifungua mkutano mkuu wa nane wa Usalama wa Raia Saccos (URA SACCOS LTD), uliofanyika jana mkoani Morogoro huku ukiwakutanisha wajumbe na wawakilishi 172 kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini.

Bwana Haule, alisema kuwa,  mbali na mafanikio makubwa kupatikana pamoja na ongezeko la akiba na amana zenye thamani ya bilioni 23.095  kutokana na ubunifu wa kujenga mtaji wa ndani pia amewaasa viongozi na watendaji kuwa waadilifu na waaminifu ili kufikia malengo makuu yaliyotokana na maadhimio ya vikao vilivyopita.

Aidha, kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Usalama wa Raia Saccos Kamishna Jenerali wa Zimamoto na Uokoaji (CGF) Thobias E.M. Andengenye, alisema kuwa, usalama wa Raia Saccos (URA SACCOS LTD),  itaendelea kutoa elimu kwa wanachama wake wote na kuendelea kujenga mtaji wa ndani kwa kununua hisa na kuweka akiba pamoja na kurejesha mkopo kwa wakati alisema.

Kamishna Andengenye, ameongeza kuwa, usalama wa Raia Saccos (URA SACCOS LTD),  itaendelea kuwahudumia wanachama wake wote ili kuwapunguzia makali ya maisha na kuwaepusha na mikopo yenye riba na masharti makubwa ili kukuza ustawi na uchumi wao na kwamba wamejipanga katika kuongeza idadi ya wanachama kupitia fursa walizonazo.

Serikali yafanya ukaguzi miradi ya miundombinu

Kaimu Mkuu wa Idara ya Miradi ya Ujenzi kutoka Baraza la Taifa la Ujenzi Injinia Wambura M. Wambura akiongea na wanahabari (hawapo pichani)kuhusu jukumu la ukaguzi wa kiufundi au kitaalam wa miradi ya ujenzi nchini jijini Dar es Salaam leo (jana).
Kaimu Mkuuwa Idara ya Miradi ya Ujenzi Injinia Wambura akiongea na wanahabari (hawapopichani) kuhusujukumu la ukaguziwakiufundi au kitaalamwamiradiyaujenzinchinijijini Dar es Salaam leo (jana).
KaimuMkuuwaIdarayaMajengokutokaBaraza la Taifa la Ujenzi Injinia Kissamo Fredrick akiongea na wanahabari kuhusu mafanikio ya Baraza hilo katika utekelezaji wa jukumu la kufanya ukaguzi wa kiufundi jijini Dar es Salaam jana (leo). (Pichana Benjamin Sawe- Maelezo).

……………..


Frank Mvungi-Maelezo
SERIKALI kupita Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) imefanya ukaguzi wa miradi mikubwa 163 yenye thamani ya zaidi ya Bilioni 2 ikijumuisha Barabara, majengo, maji na viwanja vya ndege.


Hayo yamebainishwa leo jijini Dar es Salaam na Kaimu wa Idara ya Uhandisi wa Baraza hilo Mhandisi Wambura M. Wambura alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya ukaguzi huo.Mhandisi Wambura amesema kuwa miradi yote iliyofanyiwa ukaguzi inatekelezwa chini ya ufadhili wa Serikali.

“Shughuli za kiukaguzi zilizofanyika ni pamoja na kufanya mapitio na tathmini ya michakato ya manunuzi, utekelezaji wa mikataba, utekelezaji wa miradi,ongezeko la gharama za miradi, pamoja na ubora wa kazi zilizofanyika,” alisisitiza Mhandisi Wambura.

Aliongeza kuwa lengo la kaguzi hizo ni kuhakikisha kuwa thamani ya fedha inalingana na ubora wa miundombinu iliyojengwa katika eneo husika.Aidha, Mhandisi Wambura amesema kuwa katika kipindi cha 2015/2016 baraza lilifanya ukaguzi wa kiufundi wa miradi ya matengenezo ya barabara kwa halmashauri zote za Wilaya pamoja na TANROADS kwa Mikoa ya Mbeya,Songwe,Rukwa,Katavi,Kigoma, na Shinyanga ambapo miradi hiyo iliyotekelezwa kwa fedha za mfuko wa Barabara.

Miradi mingine iliyofanyiwa ukaguzi wa kiufundi mwaka 2011 ni 14 iliyohusu ujenzi wa vituo vya afya na 36 ya ujenzi wa zahanati 50 iliyotekelezwa kwenye Halmashauri za Wilaya 20.Akizungumzia changamoto zilizobainika katika ukaguzi unaofanywa na Baraza hilo Wambura alibainisha kuwa ni kutozingatiwa kwa taratibu za kusimamia ubora wa kazi na maandalizi hafifu ya miradi katika hatua za mwanzo katika utengaji bajeti yakutosha,usanifu na ukadiriaji gharama za ujenzi.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Idara ya majengo Bw. Kissamo Elias alitoa wito kwa wadau wa sekta hiyo kulitumia Baraza hilo kufanya kaguzi katika miradi wanayotekeleza ili kuongeza tija hali itakayochochea ukuaji wa sekta hiyo.Baraza la Taifa la Ujenzi ni kitovu cha uratibu wa sekta ya ujenzi kwa taasisi zote zinazoshughulika na shughuli za ujenzi pamoja na wadau ili kuleta umoja,uwiano, na ushirikiano katika utendaji ndani ya sekta ya ujenzi,Baraza linaendelea kusimamia na kuongoza juhudi za kukuza na kuendeleza sekta ya ujenzi nchini.

Baraza la Taifa la Ujenzi ni Taasisi ya Serikali iliyoanzishwa kwa mujibu wa sheria ya Bunge namba 20 ya mwaka 1979 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2008,baraza lipo chini ya Wizara ya ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano