Saturday, May 18, 2013

HOTUBA YA MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KATIKA IBADA YA KUMTAWAZA ASKOFU JACOB ERASTO CHIMELEDYA WA DAYOSISI YA MPWAPWA KUWA ASKOFU MKUU WA SITA WA KANISA ANGLIKANA TANZANIA, KANISA KUU LA ROHO MTAKATIFU, TAREHE 18 MEI, 2013, DODOMA




Mhashamu Justin Portal Welby, Askofu Mkuu wa Canterbury na Kiongozi wa Kanisa Anglikana Duniani;
Mhashamu Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Jacob Erasto Chimeledya;
Wahashamu Maaskofu Wakuu na Maaskofu wengine;
Mheshimiwa Joseph Sinde Warioba na Mheshimiwa John Samweli Malecela, Makamu wa Rais na Mawaziri Wakuu Wastaafu, Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Mawaziri, Wabunge, Viongozi wa Ngazi Mbalimbali katika Serikali, Vyama vya Siasa na Jamii;
Viongozi wa Dini na Waumini;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;

Shukrani/Pongezi
          Naomba niungane na wenzangu walionitangulia kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa Rehema, kwa kutujalia uzima na kutuwezesha kukutana hapa katika Kanisa Kuu la Roho Mtakatifu Dodoma. Nawashukuru sana kwa heshima kubwa mliyonipa na kunishirikisha kwenye tukio hili kubwa na la kihistoria kwa Kanisa la Anglikana na nchi yetu.  Najisikia kuwa mtu mwenye bahati kubwa kuwa miongoni mwa waumini wa Kanisa la Anglikana kushuhudia Mhashamu Askofu Erasto Chimeledya wa Dayosisi ya Mpwapwa akitawazwa kuwa Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana hapa nchini.
Karibu Tanzania Kiongozi Baba Askofu Justin Portal Welby
Mkuu wa Anglikana

          Niruhusuni niungane na wasemaji wenzangu walionitangulia kumkaribisha nchini kwetu Mhashamu Justin Portal Welby, Askofu Mkuu wa Canterbury. Tunamkaribisha Tanzania na hasa Dodoma kwa furaha na upendo mkubwa. Ameipa heshima kubwa nchi yetu, jambo ambalo tutalienzi na kulikumbuka daima.  Your Most Reverend, the Archbishop of Canterbury, we warmly welcome you to Tanzania. Thank you for this big favour of coming in person to grace this auspicious occasion. We deeply appreciate this gesture of great love for the Anglican Communion and people of Tanzania.  We will always be grateful and cherish this moment.
Pongezi kwa Baba Askofu Jacob Chimeledya Kutawazwa
kuwa Askofu Mkuu

Mhashamu Baba Askofu Jacob Chimeledya;
          Kwa niaba yangu, ya Serikali na wananchi wa Tanzania nakupongeza sana kwa kuchaguliwa kwako na leo kutawazwa kuwa Askofu Mkuu wa Sita wa Kanisa la Anglikana Tanzania.  Kuchaguliwa kwako kushika nafasi hii kubwa kuliko zote katika uongozi wa Kanisa lako ni kielelezo cha imani kubwa waliyonayo viongozi wenzake na waumini wa Kanisa la Anglikana hapa nchini. Uwepo wa Baba Askofu Mkuu wa Canterbury, Mheshimiwa Justin Portal Welby, katika hafla hii ni kielelezo kingine kikubwa cha kutambulika na kukubalika kwako na  Kanisa la Anglikana duniani. Wote wanaamini kwamba unao uwezo wa kuwaongoza vyema waumini wako katika mambo ya kiroho na kimwili.  
Napenda ujue kuwa tunakupongeza kwa dhati, wakati huo huo  tunatambua kwamba majukumu yaliyo mbele yako si mepesi. Ni mazito na wakati mwingine yanaweza kuwa magumu pia. Kuna changamoto nyingi ambazo bila shaka utakutana nazo. Tunakuombea kwa Mola akuwezeshe kukabiliana na changamoto zote kwa mafanikio. Akujalie busara, subira, uvumilivu, bidii na karama za uongozi  ili uweze kumudu vyema majukumu yako mapya.  Kwa sifa ulizonazo na uzoefu wa miaka mingi katika utumishi wa Mungu na baraka zake nina imani kwamba utayamudu vizuri.  Pamoja na hayo ni wajibu wa waumini wote na kila mmoja wetu kuendelea  kukuombea kwa Mwenyezi Mungu ili akusaidie kumudu vyema majukumu mazito uliyokabidhiwa leo.
Mhashamu Askofu Mkuu Erasto Chimeledya;
          Kwa upande wetu serikalini, napenda kukuhakikishia wewe, Maaskofu wenzako na waumini wote wa Kanisa la Anglikana nchini kuwa tuko tayari kutoa kila aina ya  ushirikiano utakaohitajika kwetu. Ushirikiano tuliokuwa nao kwa muda mrefu tutauendeleza.
Niruhusu nitumie nafasi hii kumshukuru na kumpongeza Askofu Mkuu aliyekutangulia Baba Askofu Valentino Mokiwa kwa kazi nzuri aliyoifanya katika kipindi chake cha uongozi.  Uhusiano kati ya Kanisa la Anglikana na Serikali ulikuwa mzuri. Ninaamini chini ya uongozi wako, ushirikiano huo utaendelea kuimarika na kufikia upeo wa juu zaidi. 
Serikali Inathamini Mchango wa Kanisha la Anglikana
Mhashamu Baba Askofu Mkuu;
Waheshimiwa Viongozi wa Dini;
Waumini na wananchi wenzangu;
          Mimi na wenzangu Serikalini tunatambua na kuthamini sana mchango mkubwa unaotolewa na Kanisa la Anglikana kwa maendeleo ya nchi yetu na watu wake. Watanzania wengi wamefaidi na wanaendelea kufaidika na huduma  za elimu, afya, maji na nyinginezo zinazotolewa na Kanisa la Anglikana. Kwa kufanya hivi Kanisa limekuwa likiunga mkono juhudi za serikali za kuimarisha huduma za jamii na ustawi wa wananchi wake.
Nawapongeza na kuwashukuru pia kwa juhudi zenu za kuwasaidia wananchi hasa vijana na wanawake wajenge uwezo wao wa kuzalisha mali na kupunguza umaskini.  Tafadhali endeleeni kuimarisha shughuli mzifanyazo. Pia nimefarijika kusikia nia yenu ya kuanzisa Benki.  Hii ni njia muafaka ya kuwawezesha watu kupata mitaji nafuu na kwa urahisi. Nawaahidi ushirikiano wangu na wa Serikali yetu.
Ni kweli kuwa Serikali kwa upande wake imekuwa inafanya yote haya. Wahenga wanasema “Kidole kimoja hakivunji chawa”. Kwa Mashirika ya dini nayo yakichangia Watanzania wengi zaidi wakiwemo waumini wenu watanufaika na maisha yao yatakuwa bora. Muumini anayeishi kwenye lindi la umaskini ambaye hajui  atapata wapi chakula au hajui atalala wapi na kuvaa kwake ni kwa matatizo anaweza hata kukufuru kwa kuhoji  huruma ya Muumba wake ipo wapi. Tukishirikiana na tukisaidiana tutawapunguzia waumini majaribu hayo.
Viongozi wa Dini Wahubiri Upendo na Mshikamano
Mhashamu Baba Askofu Mkuu Jacob Chimeledya;
          Nakubaliana na wewe kuwa Watanzania tumekuwa tukiishi kwa amani na upendo bila kubaguana kwa rangi, kabila, dini au mahali mtu atokapo.  Waasisi wa taifa letu - Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Mzee Abeid Amani Karume na viongozi  wenzao na wale tuliofuatia tumetumia muda mwingi kuhubiri amani, umoja, upendo na mshikamano.  Dhamira yangu na viongozi wenzangu ni kuendeleza na kudumisha tunu hizo na misingi hiyo mema ya taifa letu.
          Inasikitisha na kuumiza moyo kuona kuwa wapo baadhi ya watu hawapendi kuona nchi yetu ikiendelea kuwa na amani, utulivu, umoja na mshikamano.  Hawapendi kuona Watanzania tukiishi kidugu na kushirikiana kwa pamoja katika shida na raha, nyakati za sherehe na majonzi na masuala mbalimbali ya jamii.  Wanafanya kila mbinu ili mfarakano utokee. Hivi sasa wanakazana kuchochea watu wabaguane, wachukiane na hata wauane kwa misingi ya dini zao. Serikali kwa kushirikiana na vyombo vya  ulinzi na usalama na watu wenye mapenzi mema na nchi yetu hatukubali wala hatutawaacha wafanikiwe katika dhamira zao za kishetani.
Tumejizatiti ipasavyo na tutaendelea kujiimarisha kwa kila hali kupambana na watu hao wasioitakia mema nchi yetu.  Kamwe hawatafanikiwa. Baadhi yao wameshakamatwa na kufikishwa Mahakamani.  Kazi ya kuwatafuta washirika wao inaendelea na hatutachoka mpaka wote wapatikane na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.   Ninachoweza kuahidi ni kuwa serikali haitamuonea muhali mtu, watu au kikundi cha watu kinachochezea amani ya nchi yetu na kuhatarisha usalama na maisha ya watu wake. Tutaendelea kuwachukulia hatua.  Kamwe hatuwezi kuacha maisha ya watu wetu yapotee, amani ya nchi yetu ichezewe na mtu ye yote yule kwa kisingizio chochote kile.
          Naomba viongozi wa dini muendelee kuliombea taifa. Pia muwaombee watu wenye nia mbaya wageuke kuwa watu wazuri, kama Sauli alivyogeuka kuwa Mtume Paulo. Endeleeni  kuelimisha jamii na kuhubiri amani. Hakuna mwingine anayeweza kuifanya kazi hiyo vizuri zaidi kushinda ninyi.  Ninyi mnaheshimika sana kwa nafasi mliyonayo katika jamii. Mafundisho yenu yanapokelewa kwa namna ya pekee na waumini wenu.  Tafadhali itumieni vizuri nafasi hiyo adhimu kuhimiza moyo wa upendo, amani, umoja na mshikamano miongoni mwa waumini wenu na Watanzania wote.  Hubirini tuipende nchi yetu, tuwapende jirani zetu na kila mtu ampende Mtanzania mwenzake.  Hubirini kwa uwezo wenu ili dhana ya upendo izame ndani ya mioyo yetu na akili zetu.  Tusaidiane kwenye shida na raha.  Tofauti za dini, rangi au kabila zisitufarakanishe wala kutugawa.  Tuishi pamoja kwenye nchi yetu hii nzuri tuliyopewa na Mwenyezi Mungu.
Waheshimiwa Viongozi wa Dini;
Ndugu waumini;
          Nayasema kwa msisitizo maneno haya, kwa kutambua ukweli kwamba dini zote duniani zinahimiza upendo miongoni mwa wanadamu bila kubagua. Zinawataka waumini wao kupendana na kutendeana mema, na kuwapenda na kuwatendea mema waumini wa dini nyingine. Sio kutendeana maovu. Dini zote duniani zinahubiri wanadamu kupendana, sio kuchukiana, sio kuumizana na katu hakuna dini inayohubiri kuuana. Hivyo ndivyo ilivyo kwa dini ya Kikristo, ndivyo ilivyo kwa Uislamu, ndivyo ilivyo kwa Wahindu, Budha na kadhalika. Mtu hawezi kuwadhuru wafuasi wa dini tofauti na yake eti kwa kisingizio cha kutekeleza matakwa ya dini yake. Mtu anayefanya hivyo  ana lake jambo.  Hakuna dini inayowatuma wafuasi wake kufanya maovu ya aina yoyote labda iwe dini ya Shetani.
Baba Askofu Mkuu;
Viongozi wa Dini;
Ndugu waumini na Wananchi;
          Narudia kuwaomba wanaofanya mihadhara ya dini, wahubiri dini zao bila ya  kubeza au kukashifu dini za wengine. Mimi siamini kuwa njia bora ya kumshawishi mtu akufuate ni kwa kumkashifu.  Nadhani matokeo yanakuwa kinyume chake. Zingatieni busara ya wahenga waliposema “maneno matamu humtoa nyoka pangoni”.  Kwani lugha nzuri ya kushawishi haipo? Tafadhali iondoleeni Serikali na vyombo vya dola ulazima wa kuwakamata na kuwafungulia mashtaka.
Mwisho
Mhashamu Askofu Mkuu;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
          Mwisho narudia tena kuwashukuru viongozi wa Kanisa la Anglikana kwa kunialika kuja kushiriki nanyi katika siku hii adhimu na ya kihistoria.  Nalipongeza tena Kanisa Anglikana kwa mchango mkubwa mnaoutoa kwa maendeleo ya nchi yetu na watu wake. Naomba tuendelee kushirikiana kwani sote tuna kazi moja nayo ni kuwahudumia wanakondoo wa Bwana. Mimi binafsi na Serikali ninayoiongoza nawaahidi ushirikiano usiokuwa na masharti.
          Baada ya kusema hayo, narudia kutoa pongezi zangu za dhati kwako Baba Askofu Jacob Erasto Chimeledya. Sote tunakuombea kwa Mwenyezi Mungu akushike mkono na kukuongoza katika kutekeleza majukumu yako. Nawaomba waumini wote mumpe ushirikiano kiongozi wenu ili aweze kuifanya vema kazi aliyotumwa na Mwenyezi Mungu kufanya kwenu, kwa Kanisa lake na nchi yake. Ninawatakieni nyote heri na fanaka tele katika kusherehekea siku hii tukufu.
          Asanteni.

No comments: